MABADILIKO YA KISEMANTIKI YA MANENO KATIKA LUGHA YA KIKAMBA: MTAZAMO WA KIDAYAKRONIA
Abstract
Utafiti huu ulichunguza mabadiliko ya kisemantiki ya maneno ya Kikamba kwa
mtazamo wa kidayakronia. Ulitalii jinsi maneno ya Kikamba yalivyobadilika maana
kuanzia mwishoni mwa karne ya ishirini (20) (miaka ya sabini) hadi karne ya 21. Aidha,
ulichunguza sababu za mabadiliko hayo. Uchunguzi ulifanywa kaunti ndogo ya Mwala
katika Kaunti ya Machakos ukiwalenga wazungumzaji wa lahaja ya Ki᷉masaku. Hii
ndiyo lahaja ambayo mtafiti pamoja na wakazi wengi wa kaunti ndogo ya Mwala
huzungumza. Utafiti uliongozwa na nadharia mbili: Nadharia ya Dhana ambayo
inashikilia kwamba maana ya neno ni dhana au taswira inayoibuliwa na neno hilo
akilini mwa mwanalugha wakati neno hilo linapotamkwa; na Nadharia ya Nyanja za
Kisemantiki inayoeleza kwamba maneno hayafai kuchukuliwa kama vipashio huru
vinavyojitegemea, bali yanafaa kuhusishwa na mengine yanayohusiana kimaana.
Malengo ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza nomino na vitenzi ambavyo vimebadilika
maana, kubainisha mabadiliko ya kisemantiki katika maneno hayo, kutathmini
michakato ya kisemantiki inayohusishwa na mabadiliko hayo na kuchunguza sababu
za mabadiliko hayo ya maana katika maneno ya Kikamba. Ukusanyaji wa data
ulifanywa kwa kutumia mbinu ya mahojiano na ya maktabani. Maneno yalikusanywa
kutoka Biblia za Kikamba; Mbivilia (UBS, 1974) na Mbivilia ya Ki᷉kamba kya Ivinda
Yi᷉i᷉ (IT, 2011). Vitabu vinne (4) vya Biblia viliteuliwa kwa kutumia usampuli wa
makusudi: Mwanzo na Zaburi katika Agano la Kale na Luka na Mathayo katika Agano
Jipya. Maneno mia mbili (200) yaliteuliwa kimakusudi kutoka kwenye Biblia hizi
mbili; nomino mia moja na kumi na sita (116) na vitenzi themanini na vinne (84).
Fomyula ilitumiwa kupunguza maneno haya hadi hamsini (50). Mtafiti aliteua nomino
thelathini (30) kimakusudi, kumi na tano (15) kutoka Mbivilia (1974) na kumi na tano
(15) kutoka Mbivilia ya Ki᷉kamba kya Ivinda Yi᷉i᷉(2011). Vilevile, vitenzi ishirini (20)
viliteuliwa kimakusudi, kumi (10) vikitolewa kwenye Mbivilia (1974) na kumi (10)
kwenye Mbivilia ya Ki᷉kamba kya Ivinda Yi᷉i᷉(2011). Wahojiwa walikuwa wanaume
watano (5) na wanawake watano (5) wenye umri wa miaka sabini na mitano (75) na
zaidi na wavulana watano (5) na wasichana watano (5) ambao umri wao ni kati ya
miaka kumi (10) hadi kumi na minne (14). Wote waliteuliwa kwa njia ya makusudi.
Wazee hawa walijua maana ya maneno hayo kwa kuwa wameishi katika kipindi
kinachotafitiwa na ndio mashahidi wa mabadiliko ya kisemantiki ya maneno ya
Kikamba kuanzia mwishoni mwa karne ya 20 hadi karne ya 21. Data ilichanganuliwa
kwa kulinganisha majibu ya wahojiwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo kwa
kuzingatia malengo ya utafiti. Matokeo ya utafiti huu yatawasaidia wasomaji wa matini
za Kikamba kuelewa maana za maneno kama yalivyotumika katika Biblia za awali hasa
Biblia iliyochapishwa mwaka wa 1974 na maana mpya ya maneno hayo kwa mujibu
wa Biblia iliyochapishwa mwaka 2011. Yataongezea tafiti zilizopo za kiisimu hasa
kuhusu mabadiliko ya maana ya maneno katika lugha. Ni matumaini ya mtafiti kwamba
kizazi cha sasa kitaelewa maana za maneno yanayopatikana katika matoleo ya awali ya
Biblia ya Kikamba.
Collections
- MKSU Masters Theses [146]