Mchango wa Kiswahili katika Upunguzaji wa Ajali za Vyombo vya Moto Barabarani: Mifano kutoka Madereva wa Magari na Pikipiki Tanzania
Abstract
Makala haya yanajadili mchango wa Kiswahili katika kupunguza ajali za vyombo vya moto barabarani. Tangu serikali ya Tanzania iboreshe miundombinu ya barabra baada ya uhuru, mwaka 1961, kwa kutengeneza barabara zenye upana wa kutosha na ubora wake,ilitegemewa kwamba kutakuwa na upungufu ama uondoshwaji kabisa wa ajali za barabarani. Kinyume chake, na kama inavyoonekana kwenye vyombo mbalimbali vya habari, hata baadhi ya waTanzania wamekuwa wamepoteza maisha kwa ajili ya ajali za mara kwa mara. Baadhi ya sababu zilizotolewa na mamlaka husika ni pamoja na mwendokasi wa madereva, uchakavu wa magari (vyombo hivyo), kukosa umahiri wa uendeshaji na hoja zinazohusiana na hizo. Waandishi na wataalam hawajaangazia namna matumizi ya lugha ya maelekezo yanavyoweza kuchangia katika kupunguza ajali za barabarani ambazo hupunguza nguvu kazi ya taifa lile liwalo. Madereva wa vyombo vya moto Tanzania hutumia lugha kuu mbili za mawasiliano wanapoendesha vyombo hivi yaani Kiingereza kwa madereva wachache sana na Kiswahili kwa madereva wengi. Lengo la makala haya ni kuonesha kwamba Kiswahili kina mchango mkubwa katika upunguzaji wa ajali barabarani hasa kwa kuangalia lugha za maekelezo zinazotolewa barabarani kwa madereva na hata lugha ya kuelimisha madereva wa vyombo vya moto. Vibao na maelekezo yanayotolewa barabarani baadhi yake yapo kwenye lugha ya Kiingereza, lugha ambayo madereva wengi hawaifahamu wala kujua kilichoandikwa. Makala haya inaona kwamba mabango ya maelekezo haya, vitabu vya sheria za usalama barabarani na mafunzo na semina za muda mfupi na elekezi kwa madereva, zikitolewa kwa Kiswahili, zitachangia sana kupunguza ajali za barabarani. Makala imeangazia madereva wa magari na pikipiki kwa kuwa Watanzania wengi wanatumia vyombo hivi katika usafiri na shughuli za kila siku kuliko vyombo kama ndege, boti,treni na baikeli.