Mustakabali wa Ufundishaji na Ujifunzaji wa Fonolojia ya Kiswahili kwa kutumia Uwili Lugha katika Elimu ya Juu Tanzania: Mifano kutoka Programu za Uzamili
Abstract
Tangu serikali ipanue wigo wa utoaji elimu ya juu Tanzania, hususani elimu ya Chuo Kikuu, kumekuwa na ongezeko la vyuo vikuu vinavyotoa elimu ya Juu. Ongezeko hili limechangiwa na taasisi zisizo za umma kuanzisha vyuo vikuu binafsi ambavyo hutoa shahada kuanzia za awali mpaka za Uzamivu kwa kutumia ama lugha ya Kiswahili au Kiingereza. Katika vyuo Vikuu hivi, lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika kujifunzia na kufundishia somo la Kiswahili na taaluma za Kiswahili kwa shahada za awali. Katika jitihada za kupanua taaluma za Kiswahili, baadhi ya vyuo vikuu hapa Tanzania, kama vile Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo Kikuu cha Ruaha na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vinafundisha taaluma za Kiswahili kwa lugha ya Kiswahili katika kiwango cha shahada ya Uzamili na Uzamivu. Hivyo, kozi za fasihi na isimu kama vile fonolojia, mofolojia, semantiki, sintaksia, isimu Jamii, kuyataja kwa uchache, katika ngazi za uzamili hufundishwa kwa lugha ya Kiswahili. Katika ufundishaji na ujifunzaji wa taaluma za Kiswahili kwa kutumia lugha ya Kiswahili kumekuwa na changamoto za namna Kiswahili inavyowezesha ufundishaji na ujifunzaji wa fonolojia katika ngazi ya Umahiri na Uzamivu. Lengo la makala haya ni kujadili mustakabali wa ufundishaji wa fonolojia katika ngazi ya Umahiri kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Vyuo vikuu viwili vilitumika kama sampuli ya kukusanya data na Mkabala wa Kifafanuzi na Ulinganisho zilitumika katika uchambuzi wa data. Utafiti huu utasaidia kuona aina ya maboresho yanavyoweza kufanyika hasa katika kipengele cha tafsiri za istilahi za fonolojia yanayoweza kusaidia kukuza taaluma ya fonolojia na lugha ya Kiswahili kwa ujumla kwa kuwa vitabu mbalimbali vya fonolojia (vingi) vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo huwatatiza wajifunzaji na wafundishaji. Makala yanahitimisha kwamba pamoja na changamoto za tafsiri na ukosefu wa vitabu vya rejea vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili, upo mwanga mkubwa kwamba lugha ya Kiswahili inaweza kutoa maarifa ya kutosha kuhusu taaluma ya fonolojia kwa ujumla wake.