dc.description.abstract | Upataji wa elimu na maarifa ni shughuli isiyo na kikomo katika maisha ya mwanadamu. Ili kuimarisha shughuli
hii, lengo la nne la Maendeleo Endelevu linamhitaji kila mwanafunzi kutoachwa nyuma kwenye ujifunzaji na
upataji wa maarifa. Lugha ni chombo muhimu katika ufundishaji na ujifunzaji wa somo lolote lile. Hivyo basi,
ipo haja ya kumwelekeza mwanafunzi kufikia viwango toshelevu vya umilisi wa lugha, kama chombo cha
kujipatia elimu na maarifa ya kudumu maishani. Nadharia ya umaizi mseto, iliyoasisiwa na Howard Gardner
inatambua kuwepo kwa aina tofautitofauti za vipawa katika kikundi cha wanafunzi. Vipawa hivi vinastahili
kupaliliwa na kukuzwa kwa kutumia mikakati tofautitofauti inayomshirikisha kila mwanafunzi. Naye Lev
Vygotsky anapendekeza kutumika kwa mfululizo wa mikakati ya kumwimarisha kila mwanafunzi ili afikie kilele
cha matamanio yake kielimu. Ili kuchochea ukuaji wa vipawa na kumshirikisha kila mwanafunzi kwenye somo,
mwalimu analazimika kuteuwa na kutumia mikakati kadha anapofundisha. Makala haya yanatathmini mbinu,
mikakati na nyenzo shirikishi zinazofaa kutumika katika ufundishwaji wa Kiswahili kwa lengo la kukuza kipawa
cha kila mwanafunzi darasani. Mikakati yenyewe inajadiliwa kwa kuangazia utekelezwaji wa mtaala mpya wa
elimu nchini Kenya, unaopendekezwa kutumika kuanzia mwaka 2019. Mjadala kwenye makala haya unalenga
kujenga uhusiano kati ya nadharia na utekelezwaji wake kwenye shughuli za ufundishaji na ujifunzaji wa lugha
ya Kiswahili kama wenzo wa kutimiza malengo ya kitaifa na ya kimataifa kuhusu elimu.
Maneno muhimu: ufundishaji, mikakati shirikishi, umaizi mseto. | en_US |